Habari
MIPANGOMIJI NI MHIMILI MUHIMU WA MATUMIZI BORA YA ARDHI NCHINI
- 27 Nov, 2025
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya amewataka Wataalamu wa Mipangomiji kuongozwa na Dira 2050 ikizingatiwa Mipangomiji ni mhimili muhimu wa matumizi bora ya ardhi nchini.
Mhe. Mmuya amesema hayo wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 10 wa mwaka wa wataalamu hao ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Mwanza kuanzia Novemba 27 hadi 28, 2025, huku ukihudhuriwa na zaidi ya wataalamu 250 wa mipangomiji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Mchango Wataalamu wa Mipangomiji katika kusimamia na kuweka misingi ya maendeleo ya miji nchini, ni mhimili muhimu katika kuhakikisha matumizi bora ya ardhi, uundaji wa miji salama, na ustawi wa jamii kwa ujumla” amesema Mhe. Mmuya
Amesema kuwa ukuaji wa kasi wa miji unahitaji utaalamu, dira na mipango madhubuti ili kuhakikisha ustawi endelevu wa wananchi hivyo kuwataka wataalamu kufanya tathimini ya kutosha juu ya mipangomiji ya sasa na kupata dira ya kupanga miji ya kisasa ili kufikia malengo ya Dira 2050 kwa kupanga mipango ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
“Natoa wito kwa wataalamu wa Mipnagomiji na wataalamu wengine Na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi, wakati mnafanya mipoango yenu na mnatekeleza mipango yenu mtumie Dira 2050 katika kupanga mipango mbalimbali na kutekeleza wajibu wenu” amesisitiza Mhe. Mmuya.
Aidha, Mhe. Mmuya amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa Mipangomiji kutanguliza maslahi ya wananchi kupitia mipango jumuishi na shirikishi inayozingatia changamoto za sasa kama ongezeko la watu mijini, uhaba wa ardhi, migogoro ya ardhi, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha taaluma hiyo inakua kwa kasi na kwa ufanisi ili kupata miji ya kisasa na kusisitiza kuwa mipango ya miji ikitekelezwa ipasavyo itakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na kivutio muhimu cha uwekezaji.
Aidha, Naibu Waziri ameitaka Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) kuendelea kuimarisha udhibiti wa viwango vya kitaaluma na maadili ya taaluma hiyo, sambamba na kuongeza juhudi za kuhamasisha wataalamu kutumia mbinu za kisasa, teknolojia na tafiti katika kupanga miji endelevu.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB), TP. Martha Mkupasi amesema mkutano huo ni jukwaa la kuwakutanisha wataalamu wa Mipangomiji kujadili mwenendo wa taaluma, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma miongoni mwa wataalamu kutoka sekta binafsi, taasisi za umma pamoja na kuongeza maarifa kupitia mafunzo.
TP. Mkupasi amesema kuwa Bodi itaendelea kusimamia taaluma ikiwa ni pamoja na kuandaa mafunzo mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wataalamu wa mipangomij waweze kuendana na mabadiliko ya kisasa hasa matumizi ya teknolojia na mbinu shirikishi za mipangomiji.
Mkutano huo wa siku mbili unaongozwa na kaulimbiu ya “kutoka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 hadi Uhalisia; Mageuzi ya Mustakabali wa Miji ya Tanzania” umeawakutanisha zaidi ya wataalamu, wadau wa sekata ya mipangomiji 300 kutoka katika wizara mbalimbali, mikoa, halmashauri nchini, taasisi za elimu ya juu, kampuni binafsi na wengine kutoka nje ya nchi.