Habari

MAJALIWA AZITAKA HALMASHURI KUWEKA MPANGO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA MATUMIZI YA MRADI WA LTIP

  • 19 Apr, 2024
MAJALIWA AZITAKA HALMASHURI KUWEKA MPANGO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA MATUMIZI YA MRADI WA LTIP

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote zinazotekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) kuandaa mpango wa ufuatiliaji na tathmini ili kupima ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo.

 

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo machi 22, 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mradi wa uboreshaji usalama wa miliki za ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

 

Waziri Mkuu pia amezielekeza Halmashauri zote ziandae mpango mahsusi wa kupata suhulu ya migogoro inayohusu mipaka ya vijiji. 

 

“Lengo la Serikali ni kupima ardhi yote nchini ili wananchi wakiwepo wanavijiji waweze kuitumia katika kufanya shughuli za kiuchumi, Wenyeviti wa Halmashauri hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa Timu inayotekeleza mradi ili mapungufu yaliyopo yapatiwe suluhu” 

 

“Nasisitizia wakuu Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti na watendaji katika vijiji washiriki kikamilifu kuwafikia wananchi na kuwaelimisha umuhimu wa matumizi sahihi ya ardhi, ili waweze kunufaika pamoja na kupata hati miliki za ardhi wanayoimiliki” ameeleza Waziri Mkuu.

 

Waziri Mkuu pia amewataka Watalaam wa sekta ya ardhi, kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji katika hatua zote za utekelezaji wa mradi. 

 

Amesema kuwaelimisha Viongozi hao kutawasaidia katika kuhamasisha wananchi, lakini pia kutoa elimu kuhusu masuala ya ardhi.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda, amesema mradi huo unategemea kutekelezwa katika halmashauri za Wilaya zilizoko kwenye mpaka wa kimataifa wa nchi, Wilaya zenye migogoro mingi ya matumizi ya ardhi na Wilaya zenye fursa kubwa za kiuchumi.

 

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na kasi kubwa ya ukuaji wa miji na vijiji kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu linalosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi iliyopangwa na yenye usimamizi mzuri na salama, hivyo uboreshaji wa miliki za ardhi utaenda kuwa suluhu.

 

Kwa upande wake Meneja wa Mradi Vijijini Joseph Osena, amesema kuwa Mradi huo wa Uboreshaji usalama wa milki za Ardhi unaenda kutatua changamoto nyingi za ardhi ambazo zimekuwa zikiyakumba maeneo mengi nchini.

 

Amweataka viongozi wa kijamii kutoa ushirikiano kwa team ya watekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo.

 

Naye Diwani wa Kata ya Ruangwa Halima Mponda, ameipongeza Serikali kupitia Wizaya ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa juhudi inazozifanya katika kupima vijiji hali ambayo inaenda kumaliza migogoro mingi iliyokuwa inatokea.

 

Mradi wa uborshaji wa usalama wa miliki za Adhi (LTIP) unasimamiwa na Wizara ya Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiwa na kauli mbiu isemayo Usawa wa Kijinsia katika Umiliki wa Ardhi katika ustawi wa Jamii.