Habari

MAAFISA USAJILI WASAIDIZI NI KIUNGO MUHIMU KWA WANANCHI NA SERIKALI

  • 28 Nov, 2025
MAAFISA USAJILI WASAIDIZI NI KIUNGO MUHIMU KWA WANANCHI NA SERIKALI

Maafisa Usajili Wasaidizi wa Hati wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kiungo muhimu kwa wananchi na serikali yao kwa kuwa wanajukumu la msingi la kusajili wa Hati Milki za Ardhi nchini.

 

Akizungumza na Maafisa Usajili Wasaidizi wa Hati leo Novemba 28, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa watumishi hao, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi Prisca Lwangili amewahimiza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu na kwa kuzangatia maslahi ya taifa.

 

"Ni wajibu wenu kutekeleza kazi zote chini ya kada hii kwa weledi, uadilifu na kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali kwa maslahi ya wananchi, si maslahi binafsi,” amesema Prisca. 

 

Kwa upande wake, Msajili wa Hati, Bw. David Mushendwa amesema, maafisa hao ni kiungo muhimu katika mnyororo wa usajili wa ardhi, kwa kuwa wao ndiyo huandaa na kuchambua nyaraka kabla ya kufikishwa kwa Msajili kwa maamuzi. 

“Mafunzo haya si tu kuongeza ujuzi, bali ni sehemu ya maandalizi rasmi kwa kuajiriwa. Kuyapata, hili ni eneo muhimu kuwaimarisha ili mjue mnaenda kufanya nini katika utumishi wa umma mkizingatia maadili ya utumishi wa umma, utunzaji wa nyaraka, usalama wa Serikali, miongozo ya kazi,” amesema.

 

Naye Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Dodoma Bi. Juliana Ngonyani, ameahidi kuwa ofisi hiyo itasimamia kikamilifu utekelezaji mafunzo hayo na kuhakikisha kuwa washiriki wakati wa kutekeleza majukumu yao wanazingatia sheria, kanuni na taratibu kwa matokeo bora.

 

Mafunzo hayo ni ya siku mbili ambayo yanalenga kuwajengea uwezo watumishi hao na yanafanyika kuanzia Novemba 28, 2025 na yanatarajiwa kukamilika Novemba 29, 2025 ambapo watumishi 30 wa kada hiyo wanashiriki kutoka mikoa yote nchini.