Habari

KAMISHNA WA ARDHI TABORA AMALIZA MGOGORO WA POLISI NA WANANCHI

  • 11 Dec, 2023
KAMISHNA WA ARDHI TABORA AMALIZA MGOGORO WA POLISI NA WANANCHI

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki ameumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya Jeshi la Polisi Kituo cha Nanga na wananchi waliouziwa viwanja ndani ya  eneo la jeshi hilo katika wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora.

 

Kamishna Husein Sadiki na timu yake walifika katika eneo la mgogoro tarehe 7 Desemba 2023 kwa lengo la kukutana na  uongozi na wajumbe wa serikali ya kijjji cha Nanga, Mkuu wa Kituo cha Polisi  Nanga pamoja na mtendaji aliyekuwepo wakati wa kubariki uuzwaji maeneo ya jeshi la polisi.

 

Mgogoro wa eneo hilo ulizuka kufuatia wananchi kuuziwa viwanja katika eneo la Polisi kwa madai kuwa uuzwaji huo ulibarikiwa kwa pamoja na uongozi wa kijiji cha Nanga pamoja na Ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Igunga. 

 

Akizungumza katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro huo, Diwani wa kata ya Nanga Roberth Jidai alisema, yeye kama mwakilishi wa wananchi alipelekewa hoja ya kuwa wananchi wameuziwa viwanja kwa kufuata taratibu zote lakini wanazuiwa  kufanya maendelezo kwa maelezo kuwa eneo hilo ni la jeshi la polisi jambo lililosababisha  yeye kutaka kujua zaidi kuhusu suala hilo.

 

Amesema, baada ya kufuatilia kwa undani  kwa kuiuliza serikali ya kijiji alielezwa kuwa,  uuzwaji viwanja ni mradi wa serikali ya kijiji na ulibuniwa kwa lengo la kuupanga mji sambamba na kupunguza maeneo ya taasisi yaliyo makubwa na mpango huo ulishirikisha taasisi husika  ikiwemo jeshi la polisi.

 

"Baada ya kuwa tumeapishwa nililetewa hoja hii na wananchi zaidi ya  30 wakiwa na hati za viwanja na nilitaka kujua ilikuaje na baada ya kuuliza nilielezwa na serikali ya kijiji kuwa, huo ulikuwa mradi wa serikali ya kijiji wenye lengo la kupunguza maeneo ya taasisi ambayo ni makubwa" alisema Diwani

 

Kufuatia maelezo ya uongozi wa kijiji pamoja na kukagua baadhi ya nyaraka za mauziano ya viwanja, kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Sadiki alibaini kwamba, kijiji kilikaa kikao kwa madhumuni ya kumega maeneo ya umma ambapo eneo la Polisi lilimegwa na kutolewa vipande 51 vya ardhi. Hata hivyo, upimaji wa vipande hivyo haukupata idhini na hakukuwa na mpango mji ulioidhinishwa. Aidha, baadhi ya wajumbe walikiwa ni wanufaika wa mpango huo. 

 

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki  aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, kikao kilichofanya maamuzi ya kuchukua na kuuza viwanja eneo la polisi  hakikuwa na mamlaka hayo na kilichofanyika ni batili.

 

"Kikao chao kile hakikuwa na mamlaka ya kumega maeneo ya taasisi. Maeneo yanayomilikiwa na serikali yaheshimiwe iwe kwa taasisi yoyote na hakuna kikao cha kijiji chenye mamlaka ya kusema tunamega eneo la taasisis" alisema Sadiki.

 

Mtendaji wa kijiji cha Nanga Henry Masanja alisema, kufuatia kadhia iliyotokea aliomba mamlaka zenye jukumu la kusimamia mamlaka zilizo  chini kuhakikisha zinatoa ushauri mzuri kwa mamlaka za chini  kwa kuwa kilichotokea ni ushauri mbaya kutoka mamlaka ya juu.

 

Mjumbe wa serikali ya kijiji Lawrence Kishiwa ameeleza kuwa tatizo ni wajumbe wanaochaguliwa kutopewa elimu ama semina kuhusu miiko na mipaka yao ya utendaji kazi kwa sababu wao huelezwa kuwa, wanayo mamlaka ya kugawa ardhi jambo alilolieleza linasababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu utendaji katika mamlaka wanazozisimamia.

 

Aliyekuwa mtendaji wa kata ya Nanga Ambele Mwangomo ambaye alialikwa katika kikao hicho kutokana na kuwa kiongozi wakati wa zoezi la uuzwaji viwanja alieleza mbele ya kikao hicho kuwa,  amejifunza viongozi wa serikali wanaoshirikiana na wananchi katika kutoa huduma kwa jamii wanapaswa kufuata misingi vizuri na sheria inavyoelekeza.

 

" Kwa ngazi yetu ya kama serikali ya kijiji tuliweza kutekekeza hilo lakini kutokana na kutoelewa vizuri  taratibu zinaenda vipi tuendekea kuwasiliana na mamlaka ya wilaya yaani wataalamu wa ardhi na kulisimamia hilo tukidhani tuko sahihi" alisema Mwangomo.

 

Akihitimisha kikao hicho, kamishna wa ardhi msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki amesema, ni lazima viongozi wajionye katika nafsi zao hasa pale wanaposhughulika  na mali za serikali. ''Ni hatari iwapo viongozi mliopewa dhamana mnabariki kumega na kujigawia maeneo ya umma. Ni batili. Kazi tunayoenda kuifanya ni kupitia kila mmoja anaesemekana alipatiwa eneo hili''. alisema

 

"Hatutaruhusu yeyote kunufaika na batili iliyofanyika hali ya kuwa ameshiriki katika kikao kilichoazimia kukata maeneo ya umma. Eneo la Polisi litabaki kuwa la Polisi". Alisema Kamishna Sadiki