Habari
BODI ZA WATHAMINI NA MIPANGOMIJI ZIMETAKIWA KUTUMIA MIFUMO KUBORESHA HUDUMA ZA SEKTA YA ARDHI NCHINI
- 09 Sep, 2026
Bodi ya Usajili wa Wathamini (VRB) na Bodi ya Mipangomiji (TPRB) zimetakiwa kuongeza kasi katika matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi.
Akizungumza na watumishi wa bodi hizo Septemba 8, 2026 wakati alipotembelea ofisi hizo Mtumba, Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewasisitiza watumishi hao kutumia mifumo katika utoaji wa huduma ili kuongeza kasi na ufanisi wa kazi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mmuya amewataka Watanzania wenye maeneo kuhakikisha wanafuata taratibu za kumilikishwa ardhi ili kuwa na umiliki ulio salama na kuepukay migogoro ya ardhi isiyotarajiwa.
Aidha, amezipongeza bodi ya VRB na TPRB kwa namna wanavyowasimamia wataalamu katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kuchukua hatua za kinidhamu pale wataalamu wanapokiuka misingi, kanuni na maadili ya taaluma zao.