Habari

''ANZISHENI HIFADHI ZA VIJIJI KUPITIA MRADI WA LTIP''- PINDA

  • 02 Apr, 2024
''ANZISHENI HIFADHI ZA VIJIJI KUPITIA MRADI WA LTIP''- PINDA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amevitaka vijiji vilivyopangiwa mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kuutumia mradi huo kuanzisha hifadhi za vijiji ili kutunza na kuhifadhi misitu.

 

Mhe, Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 23 Machi 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika kiwilaya kwenye halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.

 

''Namna nzuri ya kutunza mazingira kwenye maeneo yetu ni kuanzisha miradi inayoweza kusaidia kutunza mazingira na misitu kwa kuanzisha WMA katika vijiji vyenu'' amesema Mhe, Pinda

 

Amesema, vijana wanaweza kutumia hifadhi hizo za misitu zilizobainishwa na mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa kuanzisha miradi kama vile ufugaji nyuki ambapo amesema mradi huo unaweza kuwapa faida kubwa kiuchumi.

 

''Misitu yote iliyotengwa kupitia mradi wa LTIP makundi ya vijana yahamasishwe ili yaweze kufuga nyuki sisi kule kwetu tunafuga nyuki na lita moja ya asali tuko mbali kweli kweli'' amesema Mhe, Pinda

 

Mmoja wa waratibu wa mradi wa LTIP wilaya ya Kilwa ambaye ni Afisa Mipango wa Miji wa Wizara ya Ardhi Elisha Mengele alieleza kuwa, mradi wa uboreshaji usalama wa Milki za Ardhi mbali na mambo mengine umelenga  kuwa na maeneo ya hifadhi endelevu, kuondoa migogoro ya mipaka na uwezeshaji vyeti vya ardhi vya vijiji ili kuwa na nguvu ya kisheria kusimamia ardhi yao.

 

Amesema, kupitia mipango ya Matumizi ya ardhi kwenye halmashauri wilaya ya Kilwa maeneo mbalimbali yametengwa kama vile kupanga maeneo yatakayoendana na uhalisia sambamba na kuhakikisha misitu na maeneo muhimu kuhifadhiwa yanakuwepo.

 

Kwa upande wao, wananchi wa Kilwa wameonesha kuridhishwa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini kwa kuwa umewashirikisha na kutenga maeneo mbalimbali kama vile mifugo, wakulima, misitu ya asili, vyanzo vya maji pamoja na makaburi.