UMILIKISHAJI ARDHI KUONDOA CHANGAMOTO KWA WANAWAKE-NAIBU WAZIRI RIDHIWANI
Posted On: 16th May, 2022
Na Anthony Ishengoma na Munir Shemweta, WANMM MBEYA
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete
amesema faida kubwa na kipaumbele katika zoezi la Kupanga, Kupima na
Kumilikisha ardhi ni kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo
kuondoa changamoto ya akina mama kukosa nguvu ya kumiliki ardhi haki
aliyoieleza kuwa itapatikana kwa kutoa hati ya pamoja kati ya mume na
mke.
Naibu
Waziri Kikwete amesema hayo Mei 13, 2022 wakati akihutubia wananchi wa
Mbalizi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wakati wa uzinduzi wa mradi wa
Kupanga, Kupima na Kumilikishwa ardhi unaosimamiwa na Chuo cha Ardhi
Morogoro (ARIMO) na baadae kushiriki zoezi la ugawaji hati kwa wananchi
waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.
Aidha,
ameongeza kwa kusema kuwa, Kupima ardhi kutawezesha kutatua migogoro
isiyo ya razima kwa kuwa kazi hiyo inahusisha upimaji shirikishi ambao
baada ya wataalamu kujiridhisha wakati wa zoezi hilo hati hutolewa bila
ya kuwepo migogoro yoyote.
‘’Kumekuwepo
na spidi ndogo ya wananchi kwenda kuchukua hati zao lakini niwambie
ninyi kuna wakati utafika mutahitaji kulima kadiri ya taratibu za
serikali na kuepuka uharibifu wa mazingira kuna wakati itabidi zitumike
mbinu za kitaalam ili kuendelea na kilimo.’’Aliongeza Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri Wizara ya Ardhi.
Naibu
Waziri Ridhiwani alizitaja faida za kuwa na hati kuwa ni pamoja na
kuthaminiwa na kupatiwa uhakika wa kupata huduma za kibenki kwa mmiliki,
kuongeza thamani ya ardhi tofauti na ile ardhi isiyopimwa aliyoieleza
kuwa haina thamani yoyote hapa nchini.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo Ardhi Morogoro (ARIMO) Bw. Huruma Lugalla
amesema chuo chake kilikopeshwa kiasi cha Tsh. Bil 1.2 kwa ajili ya
program ya Kupima, Kupanga na Kumilikisha Ardhi kwa wakazi wa Mbalizi
mkoani Mbeya ambapo viwanja takribani 35,000 tayari vimepimwa.
Kwa
mujibu wa Lugala, kiasi hicho cha fedha walizopatiwa tayari kimewezesha
upimaji na utambuzi wa viwanja 31,06 sawa na 89% katika lengo
lililokusudiwa.
Aidha
Mkuu huyo wa Chuo cha Ardhi Morogoro, aliongeza kuwa upimaji wa viwanja
hivyo ulienda sawia na uandaaji wa michoro ya mipango miji na tayari
michoro 108 kati ya 120 ambayo ni sawa na asilimia 90% imesanifiwa na
kati ya hiyo michoro 80 imewasilishwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi wa Mkoa
kwa ajili ya idhini.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete ambaye
amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mbeya alisema zaidi ya Bil.
3 zimefika katika mkoa wa Mbeya kwa lengo la Kupima, Kupanga na
Kumilikisha ardhi na kusimamiwa vizuri na watendaji wa serikali na
kukabidhi hati kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za
kumilikishwa ardhi.